MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wameweka wazi kwamba bado hawajakata tamaa kuhusu kuweza kutetea taji lao hilo kwa msimu huu.
Jana,Mei 8, Simba iliweza kupata ushindi wa mabao 4-1 mbele ya Ruvu Shooting huku nahodha John Bocco akiwa ni miongoni mwa watupiaji akifunga bao lake la kwanza msimu wa 2021/22 kwenye ligi.
Pablo Franco,Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa bado ligi haijaisha wataendelea kupambana kupata pointi tatu.
“Unaona kwa sasa namna ambavyo ligi ipo haijaisha inaendelea nasi tuna mechi za kucheza ambapo tunatakiwa kushinda.
“Kikubwa ni utayari kwa ajili ya mechi zetu na kuona kwamba kila mchezo unakuwa na mpango tofauti kwenye kupata ushindi na hilo litatufanya tuweze kuwa kwenye sehemu nzuri ya kutwaa ubingwa,” amesema.
Simba haikuaza vema msimu huu ambapo mchezo wake wa kwanza ililazimisha sare mbele ya Biashara United, Uwanja wa Karume, Mara.
Ilipoteza kwa mara ya kwanza mbele ya Mbeya City kwa kufungwa bao 1-0 na katika mechi zake tatu za ligi hivi karibuni ilikwama kupata ushindi.