PABLO KUBADILI MBINU LEO KUIKABILI RUVU SHOOTING

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Pablo Franco, ameamua kubadili mbinu kuhakikisha kikosi chake kinarudisha furaha kwa mashabiki na kumaliza msimu vizuri, huku akianza jambo hilo katika mchezo wa leo Jumapili dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.

Katika hilo, Pablo ameamua kuunda vikosi viwili ambavyo vitakuwa na uwezo wa kucheza mechi kulingana na aina ya uwanja wanaokwenda kuuchezea.

Simba imekuwa na wakati mgumu zaidi msimu huu katika kutetea taji lake la Ligi Kuu Bara ikiwa imeachwa pointi 13 na vinara Yanga, huku ikibakiwa na mechi tisa. Yanga inazo nane.

Kitendo cha Simba kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Namungo hivi karibuni, mechi ikichezwa Uwanja wa Ilulu, Lindi, ndicho kimemfanya Pablo kushtuka zaidi

Kabla ya hapo, Simba mechi tano za ugenini nje ya Dar katika Ligi Kuu Bara ilizocheza hivi karibuni, imeshinda moja (Coastal Union 1-2), ikipoteza mbili (Mbeya City 1-0, Kagera Sugar 1-0) na sare mbili (Mtibwa 0-0 na Polisi Tanzania 0-0).

Habari zimeeleza kwamba: “Kocha ameigawa timu ili kuona anakabiliana na hali ya viwanja ilivyo, anasema kuna wachezaji wameshachoka kutokana na michezo mfululizo iliyopita, ila pia kuna baadhi wanaonekana kutohimili hali ya viwanja vibovu vya mikoani ndiyo maana sasa ameamua kubadili mbinu.

“Amesema amekuwa akiangalia kwa muda suala hilo, hivyo tayari ameamua kulifanyia ufumbuzi ili kuhakikisha hatoi nafasi kubwa ya kupoteza au kuruhusu sare mechi zijazo za mkoani.”