SIMBA imefikia makubaliano mazuri na beki wa kati anayekipiga Cape Town City ya nchini Afrika Kusini, Mkongomani, Nathan Idumba.
Idumba anasajiliwa na Simba kwa ajili ya kucheza pacha na Mkongomani mwenzake Henock Inonga ambaye ndiye beki tegemeo hivi sasa katika kikosi cha Mhispania, Franco Pablo.
Kutua kwa Idumba katika kikosi cha Simba, kutafungua njia kwa beki Muivory Coast, Pascal Wawa kutemwa katika usajili wa msimu ujao kutokana na mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Simba imefikia makubaliano mazuri na meneja na beki huyo, hivyo muda wowote atasaini mkataba wa miaka miwili ya kukipiga Msimbazi.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kutua kwa beki huyo katika kikosi cha Simba, kutaifanya safu ya ulinzi ya kati kuwa na mabeki watatu wote tishio, akiwemo Mkenya, Joash Onyango, Inonga na Idumba mwenyewe.
Aliongeza kuwa Simba imepanga kutumia dau lolote la usajili sambamba na mshahara mzuri wa kila mwezi ili kufanikisha saini ya beki huyo mwenye uwezo na uzoefu wa mashindano ya kimataifa.
“Katika misimu miwili mfululizo ambayo tumekuwa tukishiriki michuano ya kimataifa, safu ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa mengi yaliyosababishwa tufungwe mabao mengi ugenini.
“Hivyo hatutaki kuona makosa hayo yakijitokeza tena katika michuano ya kimataifa, badala yake tutaiboresha kwa kusajili beki mmoja wa kigeni mwenye uwezo na uzoefu atakayecheza pamoja na Inonga.
“Tupo tayari kutumia kiasi chochote cha fedha katika dau la usajili ili kufanikisha usajili wa beki wa kati ambaye ni Idumba. Tayari tumefikia makubaliano mazuri ambaye yeye ndiye atakayesajiliwa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alizungumzia wachezaji watakaowasajili na kuwaacha, akasema: “Lazima tufanye uboreshaji wa kikosi chetu kama kweli tunataka kufanya vizuri kimataifa.
“Wapo wachezaji watakaosajiliwa na kuachwa ambao hivi sasa ni siri yetu, kama tukiwaweka wazi tutashusha morali ya kupambana katika michezo iliyobakia, hivyo tusubirie kwanza dirisha la usajili lifunguliwe kila kitu tutaweka wazi.”