MSHAMBULIAJI MANZOKI MIKONONI MWA MABOSI YANGA

INAELEZWA mabosi wa Yanga wanamfuatilia kwa karibu mshambuliaji hatari wa Vipers ya Uganda, Cesar Manzoki, kwa lengo la kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Mshambuliaji huyo mwenye asili ya DR Congo lakini kwa sasa ana uraia wa Afrika ya Kati, amekuwa gumzo katika Ligi Kuu ya Uganda kutokana na kufanikiwa kufunga mabao 16 mpaka sasa akiwa ndiyo kinara katika orodha ya wafungaji kwenye ligi hiyo.

Manzoki ambaye ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira akiwa anatumia miguu yote katika kupiga mashuti pamoja na uwezo mkubwa wa kuruka mipira ya vichwa.

Safari yake ya soka ilianzia katika Klabu ya AS Dauphins Nours ya DR Congo ambayo alicheza kuanzia 2012 hadi 2017, kisha akatimkia AS Miniema Union ambayo alicheza kwa msimu mmoja pekee kabla ya kuchukuliwa na AS Vita mwaka 2018 hadi 2020 alipojiunga na Vipers.

Msimu uliopita katika ligi ya Uganda, mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga mabao saba pekee lakini katika msimu huu akiwa na timu hiyo tayari ameshafunga mabao 16 akiwa ndiye anaongoza kwa mabao katika orodha ya wafungaji mpaka sasa.

Taarifa za kuaminika kutoka nchini Uganda, zinasema kuwa tayari mshambuliaji huyo ameshapokea simu za mabosi wa Yanga wakiwa na lengo la kutaka kumsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu ndani ya kikosi katika michuano ya kimataifa msimu ujao ambayo inatarajiwa kuanza kati ya Septemba na Oktoba, mwaka huu.

“Ni kweli Yanga wameanza kumfuatilia kupitia baadhi ya watu wao kwa sababu Manzoki ni Mcongo, amecheza sambamba na Mayele (Fiston) na huenda akawa ndio amewashtua viongozi wa Yanga hasa kutokana na rekodi yake ya mabao ya kufunga katika msimu huu,” alisema mtoa taarifa.

Mshambuliaji huyo ambaye amekiri kupigiwa simu na viongozi wa timu kutoka Tanzania juu ya suala la kucheza Ligi ya Bongo huku akisisitiza atafutwe wakala wake ambaye anaishi nchini Ubelgiji ndiye anashughulikia suala hilo.

“Kuna kiongozi amenitafuta, tuliongea kidogo sana kwa sababu nilimwambia anaweza kuongea na wakala wangu kwa sababu yeye ndiye anajua kila kitu juu yangu lakini kwa upande wangu itakavyokuwa ni sawa kwa sababu soka ndiyo maisha yangu,” alisema Manzoki.

Chanzo: Championi.