YANGA KUMALIZANA NA KIUNGO WA BURKINA FASO

IMEELEZWA kuwa mabosi wa Yanga wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa Asec Mimosas, Stephane Aziz Ki, raia wa Burkina Faso.

Hiyo ni katika kukiboresha kikosi chao ambacho msimu ujao kitacheza Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa kitatwaa taji la Ligi Kuu Bara ama kuchukua Kombe la Shirikisho.

Yanga inadaiwa hadi hivi sasa tayari imefanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji wa timu ya taifa ya Burundi na Klabu ya Kiyovu ya Rwanda, Abedi Bigirimana.

Inaelezwa kuwa kiungo huyo amesajiliwa kwa dau la Sh 200Mil ambaye anatarajiwa kutambulishwa mwishoni mwa msimu huu.

Mmoja wa mabosi wa Yanga, amesema kuwa yapo mazungumzo yanayoendelea kufanyika kati ya menejimenti ya kiungo huyo na mmoja wa viongozi wakubwa wenye ushawishi wa usajili wa Jangwani.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 51 baada ya kucheza mechi 19 ndani ya ligi msimu wa 2021/22.