YANGA WANAHESABU NDEFU KWA AZAM FC

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa upo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Azam FC unaoatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex.

Kwa sasa Yanga inafanya maandalizi ya mwisho kabla ya kumenyana na Azam FC mchezo wa mzunguko wa pili kwa msimu wa 2021/22.

Haji Manara, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu lakini ambacho wanahitaji ni pointi tatu muhimu.

“Wachezaji wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu ujao na kila kitu kinakwenda sawa hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuweza kuona burudani.

“Haitakuwa kazi ndogo kwani Azam FC wao watakuwa nyumbani na sisi tunakwenda tukiwaheshimu wapinzani wetu ambao nao wanafanya vizuri,” amesema.

Azam FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa imekusanya pointi 28, Yanga wenyewe ni nafasi ya kwanza na pointi zao ni 48.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza walipokutana Uwanja wa Mkapa, Azam FC ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0.