TAARIFA mbaya kwa mashabiki wa Yanga ni kuwa, kiungo wao tegemeo hivi sasa, Mganda, Khalid Aucho, huenda akaukosa mchezo mgumu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC.
Hiyo ikiwa ni siku chache kabla ya timu hiyo kuvaana na Azam katika mchezo utakaopigwa Jumatano ijayo saa moja kamili usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi nje kidogo ya Dar es Salaam.
Aucho atakuwa mchezaji wa pili tegemeo kukosekana katika mchezo huo dhidi ya Azam, mwingine ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye juzi aliondolewa kwenye kambi ya Stars baada ya kupata majeraha ya nyama za paja ambayo yatamuweka nje kwa wiki mbili.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, alisema kuwa Aucho yupo katika hatihati ya kuwepo kwenye mchezo dhidi ya Azam baada ya kujitonesha maumivu ya misuli.
Kaze alisema kuwa benchi lao la ufundi limepata taarifa hizo hivi karibuni za kiungo huyo kujitonesha akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Aliongeza kuwa wakati wakikosekana viungo hao, benchi la ufundi linafurahia kuona baadhi ya wachezaji waliokuwa majeraha wanarejea ambao ni Shomari Kibwana na Chrispin Ngushi ambao walicheza mchezo wa kirafiki uliopita dhidi ya Mafunzo FC ya Zanzibar.
“Kiungo wetu Aucho aliitwa kwenye timu ya taifa ya Uganda akiwa hajapona vizuri na baada ya mazoezi na timu yake ya taifa juzi alijitonesha eneo lilelile.
“Na timu ya taifa haijampatia vipimo kujua tatizo lake hivyo atarejea nchini na kufanyiwa vipimo ili kujua ukubwa wa tatizo lake.
“Huyo atakuwa kiungo wetu wa pili muhimu katika timu huenda akaukosa mchezo ujao wa ligi dhidi ya Azam, mwingine ni Fei Toto ambaye yeye amepewa mapumziko ya wiki mbili kutokana na jeraha la goti,” alisema Kaze.