MAZINGIRA MAGUMU KWA SASA WACHEZAJI WAJILINDE,WALINDWE

KUNA namna ya kufanya hasa katika kipindi kigumu ambacho wanakuwa wanapitia wachezaji kwenye kusaka ushindi ndani ya uwanja bado wanapaswa kulindwa na kupewa kile ambacho wanastahili.

Kawaida ya wapambanaji ni muhimu kulindwa kwa kuwa wakati huu wa mzunguko wa pili mambo huwa yanakuwa tofauti na mengi hubadilika.

Tunaona kwamba wachezaji muhimu ambao ni chaguo la kwanza la mwalimu wamekuwa wakitoa machozi kutokana na maumivu ambayo wanayapata.

Hili lote linatokea pale ambapo wanapata majeraha wakati wa kusaka ushindi kwa ajili ya timu husika,machozi yao huwa mazito kwelikweli kwa kuwa yanatoka kwenye mtima wao.

Muda mwingine imekuwa ikitokea hivyo pale ambapo wakiwa mazoezini hasa pale wanapokuwa kwenye mechi za kirafiki.

Pia inakuwa muda mwingine kwenye suala la mazoezi hapa pia wachezaji wanapata majeraha hivyo bado wanahitaji kuwa salama kila eneo.

Mbali na kwamba mchezaji anapaswa kuwa mlinzi wa mchezaji mwenzake nayeye pia bado anajukumu la kuweza kujilinda katika mazingira ambayo anapitia.

Ugumu upo kwa mchezaji kurudi kwenye ubora pale anapokaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kwani kuna muda wa kuanza kusubiri upya arudi katika hali ambayo alikuwa nayo hapo awali.

Lakini ikiwa atakuwa bora muda wote inaongeza uchaguzi wa mwalimu katika kuweza kufanya chaguo kwenye kikosi cha kwanza.

Nilizungumza kuhusu suala hili wakati mzunguko wa pili unaanza kuhusu umuhimu wa kulinda afya za wachezaji kwa sababu huu ni mzunguko wa lala salama.

Wachezaji wamekuwa wakicheza kwa kukamia mechi za lala salama na mwisho inakuwa ni hasara kwa kuambulia wachezaji wengi ambao wanakuwa wanatibu majeraha.

Mpira sio vita ila ni hesabu za kusaka ushindi kwenye kila mechi ambazo timu inakuwa inacheza na hili litafanya kila mmoja afurahie.

Kuanzia shabiki,mpaka benchi la ufundi furaha yao ni kuona wanapata ushindi kwenye mechi ambazo wanacheza basi iwe hivyo kila wakati kwa wachezaji kuweza kujilinda na kulindana.

Kwa mashabiki pia wasikate tamaa kwa kuweza kuchagua baadhi ya mechi hilo sio sawa ni muhimu kujitokeza kwenye mechi zote.

Tunaona kwamba wakati huu kila mmoja anapenda kujitokeza kwa ajili ya kuweza kushangilia timu zao zikiwa zinacheza hilo linafurahisha.

Pia hata wakati Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikiwa inacheza tunaona kwamba mashabiki nao wamekuwa wakijitokeza hilo ni jambo kubwa na muhimu kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na wachezaji.

Iwe kwa wachezaji wote kufanya kazi bila kukata tamaa kwenye mechi zote na inawezekana kwa kuwa muda upo na wakati ni sasa.

Basi hata kwenye mechi za kirafiki iliyo kwenye kalenda ya FIFA matokeo yasakwe kwa udi na uvumba na itafanya furaha izidi kuwepo.

@dizo_click