UWEZO WA MAYELE WAMVUTA WINGA AS VITA

KAMA ulikuwa unahisi mshambuliaji Fiston Mayele anawapa furaha mashabiki wa Yanga na kuishia tu hapa nchini, basi utakuwa unajidanganya.

Hiyo ni baada ya Spoti Xtra kufanya mazungumzo na winga wa AS Vita ya DR Congo, Glody Makabi Lilepo ambapo ameweka wazi matamanio yake ya kutaka kucheza na Mayele ndani ya Yanga.

Mayele ambaye amejiunga na Yanga msimu huu akitokea AS Vita ya DR Congo, amekuwa mchezaji tegemeo ndani ya timu hiyo akiwa kinara wa ufungaji Ligi Kuu Bara akifunga mabao 10.

Akizungumza na Spoti Xtra, Lilepo ambaye amewahi kucheza na Mayele akiwa AS Vita, amesema: “Mayele ni mchezaji mzuri, nimecheza naye hapa AS Vita kwa misimu miwili kabla hajaondoka, tulikuwa tukielewana sana, uchezaji wetu haswa katika kumtengenezea mabao na mara nyingi alikuwa akifunga kupitia pasi zangu.

“Kwa sasa namfuatilia akiwa Tanzania na mara nyingi huwa tunazungumza, tumekuwa tukitaniana juu ya mimi kuja kucheza Ligi ya Tanzania, kwangu naamini kila kitu kinawezekana, ila kucheza na Mayele tena ni jambo ambalo natamani litokee.”

Wakati winga huyo akisema hivyo, naye mshambuliaji Kazadi Kasengu ambaye pia ni raia wa DR Congo anayecheza Tala ea El Gaish ya Misri kwa mkopo akitokea El Masry ya nchini humo, amesema: “Yanga ninaifahamu vizuri na nimekuwa nikiifuatilia, kuna wachezaji wa DR Congo wapo pale na wanafanya vizuri ila haswa Mayele ambaye amekuwa akinivutia sana uchezaji wake na ushangaliaji wake mzuri, hakika ni furaha kuwa naye katika timu moja.”