SIMBA YASAKA ATAKAYEMPA CHANGAMOTO TSHABALALA

MEFAHAMIKA kuwa Simba imeanza kumnyemelea beki katili wa kushoto anayekipiga ASEC Mimosas, Wonlo Coulibaly raia wa Ivory Coast.

Nyota huyo ambaye alicheza kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar ukiwa wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba na kuchapwa mabao 3-1, inadaiwa amewavutia mabosi wa Msimbazi hivyo wanataka kufanya jambo.

Beki huyo mwenye miaka 30, aliwahi kucheza TP Mazembe ya DR Congo pia amewahi kukipiga timu ya Taifa ya Ivory Coast ambapo hadi sasa takwimu zinaonyesha ameshacheza mechi 18.

Simba imekuwa ikitafuta mbadala ambaye atampa changamoto beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambapo mabeki kadhaa wamekuwa wakisajiliwa na kushindwa na sasa Simba wameamua kuvuka ‘boda’ kumfuata Colibaly ambaye kwa mujibu wa Mtandao wa Transfermarkt thamani yake ni euro 150,000 (Sh mil 382.4).

Coulibaly ambaye pia anamudu kucheza beki ya kulia na kiungo mkabaji, mwenyewe akizungumza kutoka Ivory Coast ameliambia Championi Jumatano kuwa, amekuwa akisikia kwa watu wake wa karibu kuwa Simba wanamfuatilia wakitaka kumsajili.

“Ni kweli Simba wanataka kunisajili lakini mpaka sasa hawajanitafuta wenyewe rasmi kusema kuwa wanataka kunisajili ila ni maneno tu.

“Pamoja na hilo haijalishi kama watakuwa tayari na ofa yao itakuwa nzuri nitajiunga nao,” alisema beki huyo mwenye urefu wa futi 5 na inchi 10.