MSUVA AITABIRIA MAKUBWA SIMBA KIMATAIFA

MCHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga kwenye kikosi cha Wydad Casablanca ya Morocco, Simon Msuva amesema kuwa kwa mwendo wa Simba wanaouonyesha kwenye michuano ya kimataifa watafika mbali.

Msuva kwa sasa anaripotiwa kuwa nchini hapa kwa madai yuko kwenye mgogoro wa kimaslahi na klabu yake hiyo ya Morocco.

Msuva amesema Simba wameshakuwa wazoefu kwenye mashindano hayo na kubwa wamekuwa na uhakika wa kupata ushindi wakiwa nyumbani na angalau hata sare wakiwa ugenini jambo ambalo ni bora kwa mpira wa Afrika.

“Simba nawaona wakifika mbali kwenye anga za kimataifa hasa kwenye mashindano haya ya kimataifa kwa sababu wana timu bora.

“Kwa mashindano ya Afrika ukiwa na uhakika wa kupata ushindi nyumbani na angalau sare ugenini, unakuwa na uhakika wa kufika mbali na Simba wanaweza kufanya hivyo.”

Simba wanashiriki Kombe la Shirikisho hatua ya makundi na ndio vinara wa kundi lao wakiwa na alama saba baada ya kucheza mechi nne inanolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco ambaye kwenye ukuta chaguo lake namba moja ni Henock Inonga.

Kesho Machi 20 inatarajiwa kuwa na mchezo wa kusaka pointi tatu mbele ya ASEC Mimosas utakaochezwa Benin na tayari viongozi pamoja na wachezaji wameshaanza maandalizi nchini humo.

Mchezo wao uliopita Uwanja wa Mkapa mbele ya RS Berkane, Simba ilishinda bao 1-0 na mtupiaji alikuwa ni Pape Sakho