WAWAKILISHI WA TANZANIA KIMATAIFA WAPANIA KUSHINDA

KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco, amesema hakuna matokeo yoyote ambayo anayahitaji zaidi ya ushindi katika mchezo wa Kundi D dhidi ya RS Berkane.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, kuanzia majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na Spoti Xtra, Pablo alisema wanatarajia kuwa na mchezo mzuri dhidi ya RS Berkane na kupata matokeo ya ushindi kwani ndio matokeo ambayo wanayahitaji kuliko jambo lolote licha ya kucheza na timu bora.

“Tunacheza na timu nzuri ambayo ilipata matokeo mazuri dhidi yetu nyumbani kwao, kwa sasa tupo nyumbani, sehemu yenye matumaini makubwa kwetu.

“Tunahitaji kupata matokeo mazuri na naamini tutakuwa na mchezo mzuri utakaotupa ushindi kwa kuwa hakuna matokeo mazuri ambayo tunahitaji zaidi ya ushindi,” alisema kocha huyo.

Pablo aliongeza kwa kubainisha kwamba, amewataka mabeki wake wakiongozwa na Joash Onyango na Inong Baka kuacha kucheza faulo zisizo za lazima karibu na goli lao ili kutowaruhusu wapinzani kufunga mabao kwa mipira iliyokufa kama ilivyotokea katika mchezo wa kwanza kule Morocco wakati Simba ikifungwa 2-0.