SIMBA YAPANIA KUWAFUNGA RS BERKANE KWA MKAPA

BARBARA Gonzalez, Mtendaji Mkuu wa Simba SC, amesema wapinzani wao RS Berkane kwenye mchezo unaoatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Jumapili hii, hawatatoka salama.

Simba inatarajiwa kumenyana na RS Berkane ya Morocco kwenye mchezo wa nne wa Kundi D, wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita ugenini kwa kufungwa mabao 2-0.

Barbara amebainisha kuwa, kwa maandalizi ambayo wameyafanya pamoja na kila mchezaji kuhitaji ushindi,

wanaamini wapinzani wao hawatatoka kwa Mkapa kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili.

“Kwa Mkapa hawatoki kwa kuwa maandalizi yapo vizuri na kila mchezaji anajua tunahitaji ushindi. Haya ni mashindano ya kimataifa na tunawakilisha nchi hivyo ni muhimu kwetu kushinda ili kuweza kusonga mbele,” amesema Barbara.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chao, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Maandalizi yetu kuelekea mchezo dhidi ya Berkane yanaendelea vizuri, tunataka kuwatahadharisha Berkane kuwa wamekuja kipindi kibaya kwa kuwa sehemu kubwa ya kikosi chetu wapo salama, tunatarajia kumkosa Chama (Clatous) kutokana na masuala ya kikanuni na Dilunga (Hassan) aliye mgonjwa.”

Tayari wapinzani wa Simba RS Berkane wameshatua Dar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo wa kimataifa.