AISHI Manula, ‘Air Manula’ kipa namba moja wa Simba ni Air Manula kwelikweli kama anavyopenda kuitwa kwa kuwa amewafunika makipa wote kwa upande wa kucheza mechi nyingi na kuwa namba moja kufungwa mechi chache.
Pongezi kubwa kwa ukuta wa Simba unaongozwa na Joash Onyango pamoja na Henock Inonga ambao umeweza kumshuhudia kipa wao akiokota mabao 6 katika mechi 15 alizocheza.
Juma amekusanya clean sheet, (cheza bila kuruhusu bao) 9 huku akiwa ameyeyusha jumla ya dakika 1,350 akiwa langoni na alikuwa akianza ni uhakika kukamilisha dakika 90.
Kipa anayefuata ni Aboutwalib Mshery wa Yanga ambaye ana jumla ya clean sheet 8 ambapo alikusanya 4 akiwa Mtibwa Sugar na sasa ndani ya Yanga pia ni 4 zipo kibindoni.
Ingizo jipya ndani ya Mbeya City, Deogratius Munish, ‘Dida’ akiwa amecheza mechi 4 mfululizo aliweza kukusanya clean sheet 3 huku ile ya nne ikigoma mbele ya Namungo FC alipoweza kutunguliwa mabao 2-0.
Dida aliweza kuhimili mikikimikiki ya Meddie Kagere wa Simba mwenye mabao matano na Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 7 kwa kuwa walipokutana uwanjani aliweza kuwa imara na aliokoa penalti mbili mfululizo ilikuwa mbele ya Simba na Ruvu Shooting.
Hizi ni rekodi baada ya mzunguko wa kwanza kukamilika hivyo kazi inaanza tena mzunguko wa pili.