KAPOMBE APEWA TUZO YA MCHEZAJI BORA

BEKI wa kazi chafu, mzawa Shomari Kapombe anayekipiga ndani ya kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco pamoja na msaidizi wake Seleman Matola ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashabiki kwa mwezi Februari.

Kapombe ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda wenzake wawili ambao aliingia nao fainali katika kuwania tuzo hiyo.

Beki wa kati Henock Inonga pamoja na wonder kid, Peter Banda ambao walikuwa wakiwania na mwisho wa siku mshindi akawa ni Kapombe.

Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Simba ikiwa kundi D na pointi 4, Kapombe amefunga bao moja na kutoa pasi mbili.

Alifunga mbele ya ASEC Mimosas kwa mkwaju wa penalti na kutoa pasi pia alifanya hivyo mbele ya USGN ya Niger katika sare ya kufungana bao 1-1.

Kwa sasa kikosi cha Simba kipo Dar baada ya kumaliza kazi ya kusaka pointi sita ugenini Niger na Morocco mbele ya RS Berkane ambapo kiliambulia kichapo cha mabao 2-0 na kusepa na pointi moja pekee.

Mchezo wao ujao ni wa ligi itakuwa dhidi ya Biashara United ya Mara unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Machi 4.