SIMBA V PAMBA, YANGA V GEITA GOLD KOMBE LA SHIRIKISHO

DROO ya mechi za Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) hatua ya robo fainali imefanyika leo Februari 21. Jumla ya timu 8 zimeweza kushuhudua droo hiyo ambayo ilikuwa mubashara pia Azam TV.
Mashabiki pia wameweza kufuatilia na sasa wanajua kwamba timu zao zitacheza na timu ipi baada ya kupenya kwenye hatua ya 16 bora.
Yanga watacheza na Geita Gold, Simba watakipiga dhidi ya Pamba hawa wote watatumia Uwanja wa Mkapa. Azam v Polisi Tanzania Uwanja wa Azam Complex na Coastal Union wakipepetana na Kagera Sugar, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa mujibu wa droo hiyo  mshindi kati ya mechi ya Yanga na Geita Gold, atakutana na mshindi kati ya Simba na Pamba katika hatua ya nusu fainali ya kwanza.
 
Mshindi kati ya Azam na Polisi Tanzania atakutana na mshindi kati ya Coastal na Kagera Sugar katika hatua ya nusu fainali ya pili.
Bingwa mtetezi wa Kombe la Shirikisho ni Simba alitwaa taji hilo mbele ya Yanga Uwanja wa Lake Tanganyika,Kigoma mwisho wa reli.
Ni kati ya Aprili 8-13 inatarajiwa kuchezwa robo fainali huku fainali ikitarajiwa kuchezwa Mei.