KAZI ya Mungu haina makosa na tunapaswa kumshukuru kwa kila jambo ambalo linatokea kwenye maisha yetu ya kila siku kwa kuwa yeye ni muweza wa kila kinachotokea.
Hakuna ambaye anaijua kesho hivyo kwa muda ambao upo kwa wakati huu kila mmoja anajukumu la kutimiza yale yanayofaa bila kuchoka.
Wanafamilia,ndugu na jamaa katika kipindi hiki kigumu ni muhimu kuzidi kushikamana tusitengane hili ni letu sote na limetokea.
Muda wa kufanya mema ni huu uliopo pamoja na kuwakumbuka ndugu jamaa na marafiki hakutakuwa na muda mwingine bali ni sasa.
Yote kwa yote kwa familia ya michezo ninatambua kwamba kwa wakati huu bado kuna maumivu ya kuondokewa kwa kijana wetu mpendwa Ally Mtoni maarufu kama Sonso.
Ni pigo kwa Watanzania kwa sababu kijana kabla ya umauti kumfikia alikuwa anatimiza majukumu ya taifa bila kuogopa na kufanya yale ambayo yanaruhusiwa kwa mujibu wa sheria.
Alikuwa miongoni mwa wale mashujaa walioshinda mabao 3-0 dhidi ya Uganda kwenye mchezo wakuwania kufuzu Afcon nchini Misri.
Kumbuka kwamba ilikuwa ni jambo ambalo lilisubiriwa kwa muda mrefu na likatimia pale Uwanja wa Mkapa.
Iliwezekana na haikuwa kazi rahisi mwisho wa siku yakatimia na furaha ya Watanzania ikawa ni kubwa kwa kuwa jambo ambalo lilisubiriwa kwa muda mrefu lilitimia.
Mbali na hilo pia alikuwa akitimiza majukumu yake vema kwenye familia yake pamoja na kuwa karibu na marafiki wake muda wote hakuna namna kwa sasa ni muda wa kuendelea kumuombea.
Mwendo ameumaliza shujaa Sonso alama ile ya upendo na juhudi inabidi viendelee kuishi kwenye mioyo ya vijana hasa katika kufanya yale makubwa na yenye manufaa kwa taifa La Tanzania.
Maisha yake alipokuwa ndani ya Kagera Sugar hakuwa mtu wa matukio mabaya bali alikuwa ni mtu wa kazi muda wote pamoja na kushirikiana na wachezaji kwa kuwa anatambua mafanikio ya timu yanabebwa na kila mchezaji.
Ikumbukwe kwamba alicheza pia Yanga ambapo huko pia kazi yake ilikuwa ni moja kutimiza majukumu ambayo anapewa na benchi la ufundi.
Moja ya mabeki ambao walikuwa wanapewa nafasi ya kuja kufanya vizuri hapo baadaye kwa kuwa alikuwa bado kijana na mwenye ndoto kubwa.
Kabla ya kucheza Yanga alikuwa ndani ya Lipuli na huko maisha yake yalikuwa ni ya aina moja upole na usikivu.
Pia alikuwa ni kiongozi imara hasa pale alipokuwa akipewa kitambaa cha kuwa nahodha wa timu hakujivunia nafasi bali alitimiza majukumu yake kwa kuwapa nafasi na kuwasikiliza pia.
Ule moyo wa kujitoa mpaka timu inapata ushindi na hata pale timu inapopoteza bado alikuwa na wachezaji na kuongea nao kwamba kesho ni yetu lazima tusikate tamaa.
Anakumbukwa kuwa miongoni mwa kikosi cha Lipuli ambacho kilitinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na kupoteza mbele ya Azam FC.
Historia yako itaishi na rekodi zako zitakumbukwa Ally Mtoni, safari yako imefika tamati mwendo umeumaliza shujaa pumzika kwa amani.
Familia yake ya Ruvu Shooting sio wao pekee bali kila mmoja ameguswa kwa ambacho kimetokea na hatuna budi ya kufanya zaidi ya kushukuru.