>

AZAM FC:UWANJA WA KARUME UNA HALI MBAYA

UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kwamba hesabu kubwa kwa sasa ni kuelekea kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Karume, Mara huku tatizo kubwa likitajwa kuwa ni ubora wa uwanja.

Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa tatizo kubwa waliloliona kwa sasa ni Uwanja wa Karume baada ya kutuma wawakilishi kuwexza kuutazama uwanja huo.

“Baada ya ushindi wa kishindo dhidi ya timu ngumu ya Baga Friends sasa Azam FC inajiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United utakaofanyika Musoma Februari 22 katika Uwanja wa Karume.

“Tuna taarifa kutoka kwa watu wetu ambao tuliwatuma kule kuangalia uwanja wametuambia kwamba uwanja una hali mbaya na haupo kwenye viwango vya kuchezea mpira lakini hatujui kile ambacho kinaendelea hivyo tunaomba mamlaka ziweze kulichukulia hatua suala hili,” amesema.

Azam FC kwenye msimamo wa ligi ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 14 na vinara wa ligi ni Yanga wenye pointi 36 baada ya kucheza mechi 14.

Inakutana na Biashara United iliyo nafasi ya 13 na kibindoni ina pointi 12 baada ya kucheza mechi 14 na huu ni mchezo wa 15 kwa timu zote ikiwa ni wa kukamilisha mzunguko wa kwanza.

Kwenye mchezo wao uliopita wa Kombe la Shirkisho mshambuliaji wao Prince Dube ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha naye alikuwa sehemu ya kikosi hicho kilichoweza kutinga hatua ya robo fainali.