NABI AKOMAA KUUNDA PACHA MPYA YA MAYELE

IMEELEZWA kuwa Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi, usiku na mchana anapambana kutengeneza uwiano wa Fiston Mayele, Heritier Makambo na Yusuf Athumani ili aweze kuwatumia pamoja.

Licha ya Yanga kuendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa na pointi zake 36, ambazo imezikusanya baada ya kucheza mechi 14, imefunga mabao 23 na sare tatu, bado Nabi haridhishwi na msimamo huo.

Chanzo chetu kutoka kambi ya Yanga iliyopo Avic Town, pamoja na safu ya Yanga kuongoza kwa mabao, bado Nabi haridhishwi na idadi hiyo, hivyo amekuwa akihaha kuhakikisha anatengeneza muunganiko wa Mayele, Makambo na Athumani, ili waweze kufunga mabao mengi zaidi.

“Pamoja na kocha kumtumia zaidi Saidi Ntibazonkiza kama msaidizi wa Mayele, naona bado analalamikia safu yake kutofunga, anasema ili kumuepusha Mayele na ile hali ya kukamiwa, ni vyema sasa akawafundisha Makambo na Athumani, namna ya kucheza pamoja.

“Kocha amesema pamoja na kuwa na mfumo wa kutumia straika mmoja zaidi, kwa sasa anafikiria namna ambavyo ataweza kuwachezesha mapema mastraika wawili ambao watakuwa wakisaidiwa na viungo kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ ili kuepusha hali ya kupata mabao machache lakini hata kumnusuru Mayele kuumizwa,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumzia hilo, Nabi alisema: “Katika timu yangu kila mchezaji ana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, lakini Mayele ndiye namba moja ambaye amejihakikishia nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

“Mara nyingi nimekuwa nikimtumia Mayele kucheza namba 9 na Fei Toto (Feisal Salum) 10 kwa lengo la kumchezesha kama kiungo, pia aanzie kukabia juu.

“Lakini bado ninaendelea kutafuta mshambuliaji mwingine atakayeweza kucheza pacha pamoja na Mayele, kama siku ikitokea Fei Toto hayupo licha ya kuwepo baadhi ya wachezaji ambao wanafanya vizuri,” amesema