BOSI SIMBA ATAMBA KUWAFUNGA ASEC MIMOSAS NA RS BERKANE

MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, ametamba kuwa, malengo waliyojiwekea msimu huu
ni kufika nusu fainali ya
Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo kwa kuanza wataanza kuchukua pointi tatu mbele
ya ASEC
Mimosas, kisha RS Berkane.


Jumapili
hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Saalaam, Simba itapambana na ASEC Mimosas, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambapo
timu hizo zipo Kundi D.


Msimu uliopita, Simba
iliishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku malengo yakiwa ni kufika
nusu fainali ya michuano hiyo
mikubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.


Akizungumza na Spoti Xtra,
Mangungu alisema kikubwa walichopanga msimu huu ni kuvuna pointi tatu katika
kila mchezo watakaocheza nyumbani kwenye Uwanja wa
Mkapa.


Aliongeza kuwa, hakuna
kitakachoshindikana kwao kutokana na maandalizi makubwa waliyoyafanya chini ya Kocha Mkuu, Pablo Franco raia wa Hispania.


“Niwaombe mashabiki wa
Simba kujitokeza kwa wingi Jumapili hii katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi
ya ASEC Mimosas
utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.

“Uwepo wa mashabijki uwanjani ndiyo chachu ya ushindi katika mchezo huo ambao muhimu kupata pointi tatu katika uwanja wetu wa nyumbani.


“Simba imekuwa
na historia ya kipee katika michuano ya kimataifa tangu miaka ya 1970, kama uongozi
tumeshakamilisha
maandalizi yote ya mchezo huo,” alisema Mangungu.