KIMATAIFA kazi inarudi ndani ya Uwanja wa Mkapa kwa Simba kuwa na kazi ya kusaka ushindi mbele ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Waliobaki kuiwakilisha Tanzania ni Simba ambao walikuwa na nafasi ya kutiga hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Haikuwa rahisi kutokana na kujiamini kupita kiasi kwa Simba baada ya kuweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa kwanza ugenini lakini wakafungwa nyumbani na kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hii ni habari mbaya kwa Simba kwamba ikiwa watajiamini kwa mara nyingine tena wanakwenda kupoteza ile tiketi ya kuiwakilisha Tanzania kimataifa kwa mara nyingine tena.
Rai yangu kwa Simba kuwa na utulivu wakati huu kwa kuwa mwendo ambao wanakwenda nao sio mzuri kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji.
Ipo wazi kwenye mechi 15 za ligi walizocheza kisha wakafunga mabao 16 sio mengi wala sio machach lakini ni lazima washambuliaji waweze kufanya tathimini upya ili kuweza kuwa bora.
Basi kwa namna ambavyo wanakwenda ni lazima wafanye kazi bora na kusaka ushindi ndani ya uwanja ili kupata ushindi na inawezekana.
Kwa upande wa ligi kwa sasa mzunguko wa kwanza unakwenda kukamilika kwa timu nyingi kwa kuwa zipo ambazo zimekamilisha tayari mpango kazi wa kwanza wa kusaka pointi tatu muhimu.
Lakini wimbo mkubwa umekuwa ni kwa waamuzi kushindwa kwenda na kasi ya mchezo hilo ni muhimu kuweza kulitazama kwa ukaribu na umakini zaidi.
Makosa yapo lakini haina maana kwamba yawe yanajirudia mara kwa mara hii naona kwamba haipo sawa nina amini kwamba waamuzi wana uwezo mkubwa na wanaweza kufanya vizuri.
Jukumu kubwa la waamuzi ni kuona kwamba wanafuata sheria 17 katika kutoa maamuzi na inawezekana kwa kuwa tunaona kwamba zipo mechi ambazo maamuzi yenu yamekuwa na matokeo chanya.
Tunakwenda kuukaribisha mzunguko wa pili kwa mechi kadhaa za mzunguko wa kwanza kukamilika hivyo ni muhimu kila mmoja kuweza kufanya kazi kwa umakini.
Mzunguko wa pili huwa na kasi kubwa kuliko mzunguko wa kwanza kwa kuwa hapa kete zote zinakamilishwa na hesabu za mwisho zinapatikana.
Itapendeza ushindani ukiendelea mpaka mwisho wa ligi kwa kuwa kila mmoja anahitaji kuona timu inapata matokeo chanya. Matokeo mazuri yanatafutwa kwa kufanya kazi na kufanya maandalizi mazuri.
Timu zote ambazo zimefanya usajili kwa mapendekezo yao binafsi wakati wa kujua masuala hayo ni sasa. Mchezo wa mpira hauhitaji mambo mengi zaidi ya vitendo na data ambazo zinaongea ukweli muda wote.
Timu zote zinatumia dakika 90 kuweza kupata maamuzi ya kile ambacho walikifanya yule atakayetumia makosa ya mpinzani wake huonekana ni mshindi na hicho ndicho ambacho mashabiki wanahitaji.
Kila mwamuzi awe makini katika kufanya kazi ya umakini katika kutimiza sheria 17 na hili inawezekana kwa kuwa wanapewa semina kila leo na hapo wanapaswa watumie vizuri yale ambayo wanafundishwa.
Furaha kubwa ya wachezaji ni kupata ushindi na furaha kubwa ya waamuzi ni kumaliza mchezo kwa uzuri bila kuleta zile kelele hilo ni jambo zuri na muhimu kuweza kufanyia kazi makosa ambayo yanatokea.
Binadamu kufanya makosa ni kawaida lakini haina maana kwamba atakuwa anarudia mara kwa mara hilo sio sawa hapo ni lazima umakini uongezeke maradufu.
Rai yangu kubwa hasa kwa waamuzi ambao ni sehemu ya mchezo na mafanikio ya mpira wetu wanapaswa wasipepese macho katika kazi yao ndani ya uwanja.
Kufanya kwao vizuri ni hazina kwa ajili ya bingwa ambaye atapatikana hapo baadaye kwa kuwa ana kazi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa hivyo atakwenda kufanya vema kwa kuwa hajabebwa.
Kusimamia kwao majukumu ambayo wamepewa kwa uzuri kutaongeza ule ushindani kufanya kila timu kupata ushindi baada ya dakika 90 bila kuwa na sehemu ya kushusha lawama.
Kila timu kwa sasa inahitaji pointi tatu muhimu hilo lipo wazi na kwa namna mambo yanavyokwenda hivi ndivyo inatakiwa kuwa mpaka mwisho wa msimu.
Kwa kupewa adhabu waamuzi hilo liwe funzo lakini zisiwe adhabu za kuwakomoa waamuzi kwa kuwa nao bado wanamajukumu ya kufanya.
Suala la waamuzi sio Tanzania hata kwenye Afcon 2021 tumeshuhudia mambo haya lakini ni lazima kujifunza na kuwa imara zaidi.