KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amefunguka kuwa benchi la ufundi la klabu hiyo halijaridhishwa na mwenendo wa ufungaji mabao ndani ya kikosi chao na tayari wamekaa na mastraika wa kikosi hicho kuangalia namna ya kumaliza tatizo hilo.
Simba msimu huu wamekuwa na changamoto kubwa kwenye safu ya ushambuliaji mpaka sasa wametupia mabao 16 kwenye mechi 15 ambazo wamecheza.
Kwenye Ligi Kuu Bara mpaka sasa kwa Simba ni Meddie Kagere pekee ambaye amefanikiwa kuandikisha mabao msimu huu akiwa tayari amefunga mabao matano, huku John Bocco na Chris Mugalu wao wakiendelea kuwa na ukame wa mabao.
Akizungumzia changamoto ya safu yao ya ushambuliaji msimu huu, kocha Matola amesema: “Kama benchi la ufundi tunakiri kuwa ni kweli tumekuwa na changamoto katika safu yetu ya ushambuliaji msimu huu, tatizo ambalo kama benchi la ufundi tunalifanyia kazi ili kuhakikisha linamalizika na tunafunga mabao.
“Tayari tumekaa na washambuliaji wetu na kuangalia wapi tunakosea ili kurekebisha, pia kuwaweka wazi kuwa hatuhitaji kuona hali hii inaendelea.”
Simba ni mabingwa watetezi wamekuwa kwenye mwendo wa kusuasua ndani ya ligi msimu huu wa 2021/22 hasa kwenye safu ya ushambuliaji kwenye mechi mbili mfululizo ndani ya dakika 180 ni mabao mawili yamefungwa.
Bao moja lilifungwa na Kagere kwa penalti mbele ya Tanzania Prisons na bao moja limefungwa na Clatous Chama mbele ya Mbeya Kwanza, Uwanja wa Mkapa.