KOCHA ALIYEWATUNGUA SIMBA APEWA TUZO

FRANCIS Baraza, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar ambaye alikiongoza kikosi chake kuitungua Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco amepewa tuzo ya kocha bora wa mwezi Januari.

Kwa mujibu wa kikao cha Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), kilichokutana hivi karibuni Dar kimechagua jina la Baraza kuwa kocha bora wa Januari.

Baraza aliwashinda Nasreddine Nabi wa Yanga na Mathias Lule wa Mbeya City yenye maskani yake Mbeya na inatumia Uwanja wa Sokoine.

Januari, Kagera Sugar ilishinda mechi mbili na ilipata sare moja iliifunga Simba bao 1-0 Uwanja wa Kaitaba na ikatoka sare ya kufungana mabao 3-3 dhidi ya Biashara United ugenini na ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.

Ushindi huo uliifanya Kagera Sugar kupanda kutoka nafasi ya 16 mpaka nafasi ya tisa.

Wengine ambao walitwaa tuzo hiyo ni pamoja na Malale Hamsini wa Polisi Tanzania,(Septemba), Nasreddine Nabi wa Yanga, (Oktoba),Salum Mayanga alipokuwa ndani ya Prisons ilikuwa ni Novemba na Melis Medo wa Coastal Union ya Tanga, ilikuwa ni Desemba.