BAADA ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania chini ya miaka 20, Tanzanite Queens kupoteza kwenye mchezo wa kuwania kufuzu tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia hesabu zimehamia kwenye maandalizi ya U 17.
Akizungumza na Spoti Xtra, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tazania, (TFF)Wilfred Kidao alisema :-“Matokeo magumu tumeyapokea lakini tumecheza na timu imara ila mpira wakati mwingine una matokeo ya kikakatili,yametufunza jinsi gani inabidi tufanye kwenye mechi za nyumbani kumaliza mechi mapema, ila hilo ni kazi ya mwalimu.
“Yote kwa yote wamerudi nyumbani ili tuweze kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo kwa kuwa hili limekwisha.Pongezi kwa mabinti hawa wamefanya jambo kubwa mpaka kufika hapa kuwa katika timu nane za Afrika sio jambo dogo jitihada zao tumeona.
“Baada ya kupokea timu leo tunakwenda kuvunja kambi tunageukia maandalizi ya U 17 tutakuwa na kikao na mwalimu kwa maana ya mikakati tunaanza kujipanga na tuna hatua tatu ambazo zitaifanya timu iweze kufuzu ambapo Afrika inawakilishwa na timu tatu na tuna nafasi kubwa ya kuweza kufanya vizuri.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Tanzania Queens, Bakari Shime aliliambia Spoti Xtra kuwa:“Tumecheza mechi salama mechi ya kwanza, (Tanzanite 1-0 Ethiopia) na mechi ya jana,(Ethiopia 2-0 Tanzanite) (juzi) lakini niwapongeze wachezaji wetu wamecheza vizuri licha ya kupoteza mechi ilikuwa ngumu na ilikuwa na ushindani mkubwa.
“Lakini kikubwa zaidi ni hali ya hewa ya Ethiopia hali ilikuwa ngumu sana nzito kwa upande wetu tulijaribu kwenda Karatu ambapo hali ya hewa ipo sawa na Addis Ababa hilo limekuwa zuri kwetu.
“ Niseme pia imechangia kwa kiasi kikubwa wachezaji wetu wamecheza vizuri na walipata nafasi nyingi nzuri zaidi ya wapinzani wetu lakini bahati mbaya wapinzani wetu wakapata bao la kutangulia na baadaye wakapata bao la pili kipindi cha pili lakini ninaweza kusema kwamba tumepiga hatua kubwa ila kwenye mashindano tumetolewa,” alisema Shime.