UONGOZI wa Klabu ya TP Mazembe, umefunguka kuhitaji kumsajili winga Mtanzania, Simon Msuva anayekipiga Wydad Casablanca ya Morocco, huku ukiweka wazi mipango yao ya kuhitaji kukirudisha kikosi chao katika mafanikio ya kimataifa kunako michuano ya Afrika.
Msuva licha ya timu yake ya Wydad Casablanca kuendelea kucheza katika mashindano mbalimbali, lakini winga huyo yupo Tanzania akiendelea kujifua, huku ikielezwa kwa sasa hayupo kwenye maelewano mazuri na mabosi wake hao kutoka Morocco.
Bosi mmoja kutoka TP Mazembe ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema kwamba, wapo kwenye mikakati ya kuhitaji kumsajili Msuva, huku akisema malengo yao ni kuja hapa nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na muhusika ambaye wanaamini kama watamsajili basi atawasaidia hususan katika michuano ya kimataifa.
“Ni kweli Msuva ni moja kati ya wachezaji ambao tumekuwa tukiwahitaji kwa muda mrefu kabla hajajiunga na Wydad Casablanca, lakini shida kubwa kwa kuwa alikuwa anacheza Morocco ilikuwa rahisi kwa yeye kuhamia
alipo sasa, lakini kwa hiki ambacho kinaendelea kati yake na timu tunaamini ni muda wetu wa kufanya naye mazungumzo.
“Tunaangalia uwezekano wa sisi kuja Tanzania kwa ajili ya mazungumzo na mchezaji mwenyewe tuone
itakuwaje.
“Msuva ni mchezaji mzuri na mkubwa, hivi sasa tunahitaji kuirudisha timu katika ubora wa kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na tunamuona Msuva akiwa katika hadhi hiyo,” alisema bosi huyo.
Mratibu wa TP Mazembe, Jean Kazadi,alipotafutwa kuzungumzia dili hilo, alisema: “Uongozi upo kazini katika kuhakikisha TP Mazembe inasajili wachezaji wazuri.
“Kuhusu Msuva sikatai kuzungumza kuwa tayari tumezungumza naye au tupo katika mazungumzo naye, lakini unatakiwa kufahamu kuwa TP Mazembe inamuhitaji kutokana na uwezo mkubwa alionao,”.