Singida Black Stars vs Mashujaa FC, KMC Complex Septemba 30

HUSSEN Masanza, Ofisa Habari wa Singida Black Stars amebainisha kuwa mashabiki katika timu hiyo wanazidi kuongezeka kwa kasi ya ajabu jambo ambalo linamaanisha kukua kwa familia hiyo.

Septemba 30 2025 Singida Black Stars itakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara ya NBC dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma Uwanja wa KMC Complex saa 8:00 mchana katika msako wa pointi tatu muhimu.

Masanza amesema: “Mashabiki wetu wanaongezeka kwa kasi ya ajabu! Kwa takwimu ambazo bado si rasmi, tunaweza kufikisha zaidi ya mashabiki milioni 10 hivi sasa na familia inazidi kukua kila siku.

“Tunawaona uwanjani, tunaona idadi ya wafuasi ikiongezeka kwenye mitandao yetu na tunaona jinsi msisimko wa mechi zetu ulivyo mitaani.

“Tumeshatangaza viingilio vya mechi yetu na Mashujaa FC kesho pale KMC Complex ni shilingi 2,000 (mzunguko) na shilingi 5,000 (VIP). Unaweza kununua popote ulipo kupitia N-Card.

“Mechi yetu kesho itachezwa saa 8:00 mchana. Ni muda mgumu kidogo kwa hali ya hewa ya Dar, lakini haitutishi. Tumewahi kucheza saa 4 asubuhi kule Tabora. Wachezaji wetu ni wapambanaji hata mechi ikipangwa saa 9 usiku, wako tayari kupambana. Kesho tukutane KMC Complex kuishangilia timu yetu dhidi ya Mashujaa FC,”.

Timu hiyo inanolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ambaye aliwahi kukinoa kikosa cha Yanga SC ambao ni mabingwa watetezi msimu wa 2025/26.