Baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Qarabağ, Benfica imefanya uamuzi mkubwa kwa kutengana na kocha wake mkuu na kumrejesha gwiji wa soka, José Mourinho.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani zilizoripotiwa na Fabrizio Romano, Mourinho amekubali ofa ya Benfica, kwa makubaliano ya mdomo yatakayomuweka pale hadi Juni 2027. Hatua za mwisho zinatarajiwa kukamilika ndani ya saa 24, huku tangazo rasmi likisubiriwa muda wowote.
🚨🦅 BREAKING: José Mourinho kwa Benfica, here we go! “Special One” anarudi rasmi nyumbani na kandarasi ya miaka miwili tayari kwa ajili yake.
Hii itakuwa mara ya pili Mourinho kuinoa Benfica. Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2000/2001 mwanzoni mwa maisha yake ya ukocha, ambapo alidumu kwa miezi minne tu na kusimamia michezo 10: akishinda mitano, kutoka sare mitatu na kupoteza miwili.
Kazi yake ya mwisho ilikuwa na Fenerbahçe ya Uturuki, ambapo hakufanikiwa kushinda taji la ligi wala kuipeleka timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa. Sasa, akiwa na umri wa miaka 62, Mourinho anakabidhiwa jukumu la kuirejesha Benfica kileleni mwa soka la Ulaya na ndani ya Ureno.
Kwa mashabiki wa Benfica, huu si usajili wa kawaida tu — bali ni tukio la kihistoria linalomrudisha mmoja wa makocha maarufu zaidi wa Ureno katika dimba la Estádio da Luz.