YANGA SC YAKOMBA MILIONI 262.5 KUTOKA SportPesa

 KAMPUNI ya SportPesa imewapa Yanga SC Milioni 262.5 ambazo ni sehemu ya kukamilisha takwa la kimkataba kwa kutoa gawio la Tsh milioni 262.5 kama sehemu ya hongera kwa mafanikio bora yaliyopatikana ndani ya timu hiyo. Ilikuwa Julai 9 2025.

Ikumbukwe kwamba Klabu ya Yanga SC imekuwa na mahusiano ya muda mrefu yanayokaribia kufikia miaka 8 na Kampuni ya SportPesa ambao ni wadhamini wakuu wa Yanga SC katika kipindi hiko chote.

Miaka hiyo 8 inagawanyika katika vipindi viwili. Mkataba wa kwanza wa SportPesa na Yanga SC ulikuwa wa miaka mitano ambao ulimalizika mwaka 2022 ukiwa na thamani ya Bilioni 5.2.

Mwaka 2022 SportPesa na Yanga SC waliingia mkataba mwingine wa miaka mitatu wenye thamani ya Bilioni 12.33, ambapo kwenye kila msimu Yanga SC wamekuwa wakivuna kiasi cha Shilingi Bilioni 4 ambazo zimekuwa zikitumika kwa maendeleo ya timu hiyo.

Katika kipindi cha miaka 8 umeifanya Yanga kuvuna zaidi ya Bilioni 17. Hii imefanya timu hiyo kuwa na jeuri ya kununua mastaa wakubwa kama Aziz Ki, Chama Clatous, Pacome.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba amesema: “Sportpesa tunachukua nafasi hii adhimu kuwapongeza sana Viongozi wa Young Africans SC kwa namna ambavyo wameibadilisha hii Klabu. Young Africans SC imepata mafanikio kwenye msimu ambao ulikuwa mgumu sana. Kubeba mataji matano sio jambo dogo kabisa katika historia ya nchi hii.

“Huu ndio mwaka bora kabisa katika historia ya Klabu hii. Kwenye mkataba wetu tulikubaliana kuwa na zawadi ya gawio kama sehemu ya matokeo haya ya kuwa na msimu bora na wenye mafanikio. Leo tutakabidhi hundi ya Tsh 262.5m kwa Young Africans SC kwa kufikia mafanikio haya. Kampuni ya SportPesa kwa kipindi cha miaka saba hatujawahi kukosa kutimiza sharti letu la kimkataba.

“Watanzania wana matamanio makubwa ya kuleta kombe la Afrika. Kwa Uongozi huu sina mashaka kuwa hili linawezekana. Young Africans SC ina Wachezaji bora kutoka kila kona la bara la Afrika. Niwatakie kila la kheri kwa msimu unaokuja na misimu mingine.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.