Mchezaji wa soka wa kimataifa kutoka Ghana, Bernard Morrison, ametoa andiko la kugusa moyo kupitia ukurasa wake rasmi, akieleza safari yake ya mateso kutokana na jeraha la goti ambalo lilimweka nje ya uwanja kwa karibu mwaka mmoja. Katika andiko hilo, Morrison amewashukuru watu mbalimbali waliomsaidia katika kipindi hicho kigumu cha maisha yake ya soka na kuweza kumrudisha uwanjani.
Morrison alianza kwa kueleza kuwa tangu mwezi Januari 2024, aliporejea Tanzania kwa ajili ya matibabu ya goti lake, alikumbana na changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa huduma sahihi na ucheleweshwaji wa matibabu sahihi, hali iliyosababisha kuendelea kwa maumivu kwa muda mrefu.
Baada ya vipimo vya MRI, aligundulika kuwa na tatizo kubwa la “Meniscus Grade 3 Tear”, lakini daktari aliyemfanyia upasuaji wa awali hakulishughulikia ipasavyo. Morrison aliuita upasuaji huo kuwa wa “kipuuzi” na kusema daktari huyo alitumia goti lake kama “mechi ya kirafiki”.
Hata hivyo, kupitia msaada wa watu wachache wenye nia njema, Morrison aliweza kusimama tena. Akiwataja kwa majina, Morrison amesema:
🟢 “Mheshimiwa Hamis Mwinjuma (Mwana FA) alionyesha upendo na kujali kwa kunisaidia kuunganishwa na watu waliowezesha matibabu, akiwemo Mr. Ndama na Mr. Kitumbo wa Tabora United.”
🟢 “Mr. Salim Abdallah ‘Try Again’ alilipia gharama ya upasuaji, akiwa miongoni mwa waliohakikisha nimepata huduma bora. Martin Arthur (Kofi Kinaata) naye alichangia gharama ya upasuaji.”
🟢 “Daktari Edwin Kagabo na physiotherapist Hamisi Kimweri walinipa matumaini, tiba na msaada mkubwa bila hata kuwa na mkataba wowote nami.”
🟢 “Mr. Kenneth, mmiliki wa KenGold SC, ndiye aliyenipa nafasi ya pili ya kurejea uwanjani – nafasi ambayo leo inanifanya nicheze tena mpira wa ushindani.”
Morrison alieleza pia kuwa licha ya maumivu yaliyoendelea hata baada ya upasuaji, alijitahidi kuvumilia na kufanya mazoezi kwa bidii hadi alipoanza tena mazoezi ya mpira mwezi Machi 2025.
“Sijui ningekuwaje leo kama si nyinyi,” alisema Morrison kwa hisia kubwa, akihitimisha kwa kusema:
“Asante sana. Mungu awabariki nyote kwa wema wenu. Niko tena uwanjani kwa sababu ya upendo wenu.”