AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa kwa sasa ni zamu ya mpinzani wao RSBerkane kufungwa kwa kuwa kila ambaye aliwafunga walipokutana uwanjani nao walilipa kisasi kwa kuwafunga wapinzani wao.
Mei 25 2025, Simba SC itakuwa na kazi kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni fainali ya pili baada ya ile ya kwanza iliyochezwa Morocco ubao kusoma RS Berkane 2-0 Simba SC.
Ally amesema kuwa Simba imeshafanya maajabu mengi sana kwa nyakati za sasa mbali na yale ya zamani kwa kuwa msimu huu kila aliyewafunga nao walimfunga.
“Berkane ameshamaliza zamu yake sasa ni zamu yetu. Hatuzungumzi haya sababu ya historia bali ubora ambao tupo nao. Tunakubali Benjamin Mkapa ndio ngome yetu lakini hatushindi sababu ya uwanja, tunashinda sababu ya ubora wetu. Uwanja wa Amaan ndio ulitupeleka fainali na sasa ndio utatupa ubingwa. Hatukumaliza deni na Hayati Rais Mwinyi na sasa tunakwenda kulipa deni mbele ya mtoto wake, Rais Hussein Mwinyi. Tunataka kulipa hili deni.
“Tunafahamu kuna watu wanafanya kila hila Mnyama asichukue ubingwa lakini ifanye kwa kificho, tukikuona hatutakuacha salama. Hapa tulipo tumevua kabisa vazi la utu, tumevua vazi la ustaarabu. Hapa tumelipo tumevaa unyama kwelikweli, tusitafutiane lawama. Hatutamuonea mtu aibu, tutakuharibia mazima.
“Sisi tumeshatabiriwa na Hayati Rais Dkt. Magufuli kwamba sisi ndio tutakuwa wa kwanza kuleta ubingwa wa Afrika twendeni tukakamilishe ndoto hiyo, twendeni tukachukue ubingwa wa Afrika. Makombe ya ndani tumeshashinda sana lakini sasa tunalitaka hili kwa mara ya kwanza.
“Tuko tayari kumfurahisha mama yetu Rais Dkt. Samia kwa mchango mkubwa ambao anatupatia, ametoa ndege bure kutupeleka Morocco na amekuwa akitoa motisha kwa kila mechi. Kilichobaki ni kumheshimisha mama yetu kwa kumpa kombe la Afrika na kuwa Rais wa kwanza Tanzania kubeba kombe la Afrika na tutapeleka kombe Ikulu. Wachezaji wetu waende wakapambane wanavyoweza Simba tuchukue ubingwa, watoe maarifa yao yote, watoe nguvu zao zote Simba tuchukue ubingwa siku ya Jumapili.”
Simba SC ili itwae ubingwa wa Afrika inapaswa kushinda mabao 3-0 kwenye mchezo wa Jumapili kwa kuwa tayari wapinzani wao RS Berkane wametanguliza mguu mmoja lilipo kombe kutokana na ushindi ambao walipata walipokuwa nyumbani.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.