WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC hesabu kubwa ni kuona wanapata matokeo kwenye mchezo wa fainali utakaotoa maamuzi ya mshindi wa taji hilo baada ya kete ya kwanza kupigwa ugenini, Mei 17 2025.
Hassan Dalali, Mwenyekiti wa zamani wa Simba SC ameweka wazi kuwa malengo makubwa ni kuona kwamba wanatajwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kupindua meza mbele ya wapinzani wao RS Berkane.
Mei 25 2025 Simba SC chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya RS Berkane ikiwa na kumbukumbu za kupoteza fainali ya kwanza kwa ubao kusoma RS Berkane 2-0 Simba SC. Ili Simba SC itwae taji la Afrika inapaswa kushinda mabao 3-0.
Dalali amesema kuwa hawapo tayari kuona kwamba wanashindwa kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwenye mchezo wa pili dhidi ya RS Berkane unaotarajiwa kuchezwa Mei 25 2025, Uwanja wa New Amaan.
Dalali amesema: “Mwaka 1993 mgeni alikuwa Mwinyi kikombe kikaondoka, Jumapili mgeni tena Mwinyi alafu kikombe kiondoke hatukubali. Simba tunawakilisha nchi, mtu akitufanyia ubaya anahujumu nchi.
“Vijana hili kombe wanalitaka. Tuwape ushirikiano kwa kuwashangilia muda wote uwanjani. Tuna timu nzuri sana njooni tushangilie timu yetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu na sisi huu uwe mwaka wetu.”
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.