SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetangaza kuipatia klabu ya Simba ndege itakayoipeleka timu hiyo Morocco kwenye mchezo wa kwanza wa fainali ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco itakayopigwa Mei 17, 2025.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi ametangaza uamuzi huo kwa niaba ya Serikali leo Mei 08, 2025 Bungeni Jijini Dodoma kama jitihada za Serikali za kuipunguzia Simba umbali wa safari na uchovu, Simba SC kwenda Morocco kwa ndege ya abiria kungewafanya wazunguuke na kutumia muda mwingi njiani kutokana na kulazimika kupita nchi tofauti tofauti kwa ajili ya kuunganisha ndege.
“Baada ya mafanikio makubwa ya Simba na sasa inaingia kwenye mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho linaloandaliwa na CAF, Simba inakwenda Morocco kupambana na RS Berkane na Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dr Samia imefanya maamuzi ya kutoa ndege itakayoipeleka Klabu ya Simba Morocco kwa ajili ya mchezo huo”— amesema Prof. Kabudi.