UONGOZI wa KMC umeweka wazi kuwa kwa namna yoyote ile utawazuia Simba SC kuvuna pointi tatu kwenye mchezo wa mzunguko wa pili unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex.
Ikumbukwe kwamba awali mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Mei 11 2025 ulipangwa kuchezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora na maandalizi yalianza kufanyika.
Umerejeshwa Dar, Uwanja wa KMC Complex baada ya KMC wenyewe wenyeji wa mchezo huo kuomba hivyo kwa kuwa kanuni inawapa chaguo la kuchagua uwanja wanaotaka kutumia kwa mchezo mmoja nje ya sehemu ambayo wanatumia na wana uwezo wakurudisha kutokana na sababu mbalimbali.
Khalid Chukuchuku, Ofisa Habari wa KMC ameweka wazi kuwa waliamua kupelekea mchezo huo Tabora kwa mujibu wa kanuni na wameamua kuurudisha mchezo wa Dar kwa maslahi ya mpira wa Tanzania kwa kuwa wapinzani wao Simba SC wanawakalishia nchi kwenye mechi za kimataifa.
Ikumbukwe kwamba Simba SC inapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ina kibarua cha kucheza mchezo wa hatua ya fainali dhidi ya RS Berkane ya Morocco Mei 17 ikiwa ni fainali ya kwanza na ile ya pili inatarajiwa kuchezwa Mei 25, Dar itaamua nani atasepa na taji hilo.
Chukuchuku amesema wanatambua umuhimu wa mchezo wao dhidi ya Simba SC na wamefanya maandalizi mazuri kupata matokeo mbele ya mpinzani wao.
“Huyu ni mpinzani wetu na kurudisha mchezo wetu Dar ni kwa maslahi ya mpira wa Tanzania hasa ukizingatia kwamba wanacheza mechi za kimataifa kuna faida ya timu nne kuwakilisha Tanzania kwenye mechi za kimataifa kulingana na hilo tukaomba kurudisha mchezo wetu Dar na ombi letu limekubaliwa.
“Katika mchezo wetu tupo tayari kuwakabili wapinzani na malengo makubwa ni kupata pointi tatu hilo linawezekana kwa kuwa wachezaji wapo tayari na maandalizi yapo vizuri.”
Kwenye msimamo wa ligi, KMC ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 30 baada ya mechi 27 safu ya ushambuliaji imetupia mabao 22 na ukuta ukiwa umeruhusu mabao 39.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.