NI mbinu za Kocha Mkuu Fadlu Davids anayekinoa kikosi cha Simba zimejibu wakipata ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni mzunguko wa pili kwenye ligi namba nne kwa ubora Uwanja wa KMC, Complex.
Katika mchezo huo ni Ellie Mpanzu alifungua akaunti ya mabao dakika ya 15, Jean Ahoua akatupia mabao mawili dakika ya 21 na 45 huku Steven Mukwala akifunga bao moja dakika ya 47 akiwa ndani ya 18.
Kiungo Kibu Dennis amefunga mabao mawili kwenye mchezo na bao lake la kwanza ni dakika ya 54 kwa pigo la kichwa akiwa ndani ya 18 na bao la pili katupia dakika ya 69.
Ikumbukwe kwamba Kibu D mara ya mwisho kufunga kwenye ligi ilikuwa katika mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Novemba 5 2023 baada ya dakika 90 ubao ukasoma Simba 1-5 Yanga baada ya hapo hakufunga bao kwenye mchezo wa ligi.
Hatimaye Machi 14 2025 Kibu kapachika mabao mawili akitoa pasi mbili za mabao kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ambao unafuta ile gundu ya nyota huyo chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu kukwama kufunga.
Dodoma Jiji inabaki na pointi 27 kwenye msimamo huku Simba ikiwa imefikisha pointi 57 baada ya kucheza jumla ya mechi 22 msimu wa 2024/25.
Kibu amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo baada ya dakika 90 kugota mwisho akiwa kahusika kwenye mabao manne kati ya sita yaliyofungwa na Simba huku Ahoua akifikisha mabao 12 ndani ya ligi ni kinara wa utupiaji.
Vinara wa ligi ni Yanga wenye pointi 58 kibindoni na safu ya ushambuliaji imetupia mabao 58 ndani ya msimu huku washambuliaji wake wawili Prince Dube na Clement Mzize wakiwa na mabao 10 kila mmoja.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.