MWAMBA wa Lusaka Clatous Chama kiungo wa Yanga amerejea uwanja wa mazoezi baada ya kuwa nje kwa muda kwa kuwa hakuwa fiti.
Chama alipata maumivu ya mkono katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe uliochezwa Desemba 14 2024 na ubao ukasoma TP Mazembe 1-1 Yanga.
Bao la Yanga lilifungwa na Prince Dube dakika ya 90 baada ya hapo akawa nje kwa muda mpaka 2024 inagota mwisho hakuonekana uwanjani katika mechi za ushindani.
Kwa sasa amerejea na kuanza mazoezi ikiwa ni tayari kwa majukumu ya mechi zijazo ndani ya kikosi cha Yanga.
Kwenye Ligi Kuu Bara amecheza mechi 11 akikomba dakika 486 kafunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao.
Kwa mujibu wa Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa Chama yupo tayari kwa ajili ya mechi zijazo na atakuwa sehemu ya msafara wa kikosi cha Yanga utkaosafiri kuwafuata wapinzani wao Al Hilal kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Clatous Chama amerejea na ameanza mazoezi na wachezaji wengine tayari kwa ajili ya mechi zetu zinazofuata. Tunatarajia kuwa atakuwa kwenye msafara wa kikosi kinachotarajiwa kuondoka Dar Alhamis kwa ajili ya maandalizi ya mwisho dhidi ya Al Hilal.”
Ratiba inaonyesha kuwa Januari 15 2025 itakuwa ni Al Hilal v Yanga ambapo Yanga watakuwa ugenini nchini Mauritania ngoma inatarajiwa kupigwa saa 4:00 usiku na kete ya mwisho katika hatua ya makundi itakuwa ni Yanga v MC Alger hii itapigwa Uwanja wa Mkapa Januari 18 2025 saa 10:00 jioni.