YANGA: TUNA KILA AINA YA SILAHA, MKIJICHANGANYA KAZI IMEISHA

MABINGWA mara 30 wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga wamebainisha kuwa wana kila aina ya silaha za mashambulizi kwa wapinzani wao hivyo wakijichanganya watambue kwamba watamalizwa mapema.

Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi Yanga ilitwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 ikimaliza na pointi 80 kibindoni baada a kucheza mechi 30 na imeanza msimu wa 2024/25 kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii mbele ya Azam FC kwenye mchezo wa fainali iliyochezwa Agosti 11 Uwanja wa Mkapa.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amebanisha kuwa wanasilaha nyingi kwenye eneo la wachezaji jambo ambalo linawapa ushindi kwenye mechi zao hivyo wale ambao watajichanganya watakutana na kazi nzito uwanjani.

Miongoni mwa viungo waliopo Yanga ni Mudathir Yahya, Clatous Chama, Maxi Nzengeli, Pacome, Aziz Ki.

“Kila mchezaji ni silaha ya kocha Gamondi ya ushindi kulingana na mchezo ambao tunakwenda kucheza hivyo wapinzani wetu wanapaswa kuwa makini waapokuja kucheza na sisi tunatambua kwamba ushindani ni mkubwa jambo ambalo linafanya tuwe na maandalizi mazuri.

“Iwe ni kwenye eneo la ushambuliaji, kiungo tupo imara kikosi kina wachezaji wenye ari na ushirikiano mkubwa hivyo ni muda wa kuendelea kuwapa furaha mashabiki huku tukifuata mafanikio ambayo tunahitaji kuyafikia kitaifa na kimataifa.”