SIMBA NA MATUMAINI KIBAO KWA WACHEZAJI WAO

LICHA ya wachezaji wa Simba kutokuwa kwenye mwendo mzuri katika mechi za Ngao ya Jamii ungozi wa Simba umebainisha kwamba watakuwa bora katika mechi za ushindani kwa kuwa kuna vitu vidogo wamekosa vitafanyiwa kazi.

Timu hiyo iliweka kambi Misri imepishana na taji la Ngao ya Jamii ikigotea nafasi ya tatu huku nafasi ya nne ikiwa mikononi mwa Coastal Union ya Tanga.

Kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya tatu uliochezwa Uwanja wa Mkapa Agosti 11 ni bao pekee la Saleh Karabaka dakika ya 10 lilitosha kuwapa ushindi Simba licha ya kukosa nafasi za wazi kwa wachezaji wake wakiongozwa na mshambuliaji Joshua Mukwala.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wana amini watafanya vizuri kwa kuwa timu wanayo na wachezaji ni bora.

“Unaona kwamba taratibu wachezaji wanazidi kuimarika kwenye mechi za mwanzo bado kuna vitu vidogo vinafanyiwa kazi tunaamini kwamba watakuwa imara na uzoefu wakipata basi watafanya kazi kubwa na kuwapa furaha Wanasimba.

“Eneo pekee ambalo linapaswa kufanyiwa maboresho kidogo ni eneo la ushambuliaji hilo Wanasimba msiwe na mashaka viongozi wanafanyia kazi hivyo kila kitu kitakuwa sawa.”

Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza Agosti 16 ambapo Simba watatuma Uwanja wa KMC kwenye mechi za nyumbani kwa msimu wa 2024/25.