TFF YALAANI MWANDISHI KUPIGWA BAADA YA FAINALI NGAO YA JAMII

Kufuatia picha inayotembea mitandaoni ikielezea Mwandishi wa Habari kudai kupigwa baada ya mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limelaani kitendo hicho kwa vile mpira wa miguu si sehemu ya vitendo vya uvunjifu wa sheria huku likiamini katika mchezo wa kiungwana ndani na nje ya uwanja.

Taarifa ya Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha TFF imebainisha kuwa Shirikisho hilo linafanyia kazi kubaini ukweli wa tukio hilo, na wote watakaobainika kwenda kinyume na taratibu za TFF katika usimamizi wa matukio yake watachukuliwa hatua kali.

Aidha, TFF imesema inatambua umuhimu wa Waandishi wa Habari katika kukuza michezo, hivyo itaendelea kuwapa ushirikiano kuhakikisha wanafanya kazi yao vizuri na kwa weledi.