LEGEND kwenye masuala ya uandishi wa habari za michezo Bongo kitaifa na kimataifa, Saleh Ally wengi wanapenda kumuita Jembe ameweka wazi kwamba ni muhimu Simba kumalizana vizuri na mchezaji wao Aishi Manula.
Manula hayupo kwenye mpango na Simba kwa msimu wa 2024/25 jambo ambalo lilipelekea asitambulishwe kwenye kikosi siku ya Simba Day, Agosti 3 Uwanja wa Mkapa.
Ikumbukwe kwamba Manula mkataba wake na Simba bado ni hai na haujavunjwa ambapo unatarajiwa kugota mwisho 2025 hivyo ana mwaka mmoja kuwa mchezaji wa Simba.
Jembe amesema: “Manula ni mchezaji mwenye historia nzuri na Simba kafanya kazi kubwa kwenye kutimiza majukumu yake unaona hata kwenye timu ya taifa alikuwa anaitwa akiwa anatokea Simba hivyo sio mchezaji wa kumuacha kwa mtindo ambao wanafanya Simba kwa sasa.
“Akiwa na timu ya taifa amedaka kwenye mashindano makubwa Afrika AFCON kuna Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo ni kipa anayestahili heshima na kazi yake imeonekana, kwa wakati huu ikiwa Simba hawana mpango naye ni muhimu kumalizana naye vizuri kwani haya yanayotokea sio afya kwa mpira wa Tanzania.”
Ni Ayoub Lakred, Ally Salim, Camara na Hussen Abel hawa wapo ndani ya Simba kwenye eneo la walinda mlango kwa msimu wa 2024/25.