MIFUGO FC MABINGWA LIGI 2024

TIMU ya Mifugo FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Ngende Cup 2024, kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mungurumo FC katika mchezo uliochezwa Uwanja wa michezo wa Halmashauri ya Wilaya Liwale mkoani Lindi.

Mchezo huo ambao ulikuwa na mashabiki wengi kutoka viunga vya Liwale uliochezwa Wikiendi hii ulianza kwa kasi kwa kila timu kuwa na shauku ya kuibuka na ushindi.

Mifugo ilionekana kuipania mechi hiyo kwa kupata bao la kuongoza dakika ya 30 tu kupitia kwa Rashidi Parasata ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Parasata aliwawezesha mabingwa hao kupata bao la pili dakika 56, na kufufua matumaini ya kutwaa taji hilo zaidi.

Mabingwa hao walipata bao la tatu dakika ya 70, likifungwa na Saidi Tembo, huku la kufutia machozi la Mungurumo likifungwa na Zakaria Majura dakika ya 80.

Akizungumzia mchezo huo, Nahodha wa Mungurumo, Haikosi Mpwate alisema mechi hiyo ilikuwa mgumu toka dakika za mwanzo, hivyo wakakosa kutumia nafasi ambazo walizipata hadi kupelekea kupoteza.

Wadhamini wa ligi hiyo ambao ni Tico Foundation wakiwa na lengo lake kutaka kuibua vipaji na kuviendeleza ili kuweza kutimiza ndoto zao.

 Mratibu wa mashindano hayo, Shomari Ngunduli alisema michuano hiyo imelenga kuibua vipaji vya wachezaji ambao wameonesha uwezo wao.

Mifugo wamejinyakulia Kikombe na fedha Sh. 1,000,000 wakati mshindi wa pili, akijipatia Sh. 500,000 na mshindi wa tatu ambao ni Home Boys akijipatia Sh. 200,000.

Zawadi zingine ni kwa kipa bora akitokea timu ya Mifugo, Saidi Kaseja amejipatia gloves pea moja, kocha bora toka Mifugo pia, Alex Mande Sh. 100,000.

Huku mfungaji bora ni Rehemani Mtipa na Huseni Mchite wakiwa wamepachika mabao 10 kila mmoja wamejipatia pea ya viatu moja.

Mchezaji bora wa mashindano ni Hamisi Kilwanda kutokea timu ya Mungurumo amejipatia mpira mmoja na kikundi Cha ushangiliaji bora kutokea Klabu ya Cassino FC wakijipatia Sh.100,000.

Timu zilitinga hatua ya nusu fainali zilikabidhiwa jezi seti moja na mpira mmoja ambazo ni timu Mabingwa Mifugo, Mungurumo, Home Boys na Cassino.