>

MKUDE ATINGA MAZOEZINI YANGA KWA KAZI

KIUNGO mkabaji wa Yanga, Jonas Mkude rasmi amewasili mazoezini kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake na timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.

Mkude aliibuka hapo Yanga msimu wa 2023/24 akitokea Simba baada ya kupewa mkono wa Thank You na mabosi hao wa Msimbazi.

Taarifa zilikuwa zinaeleza kuwa huenda nyota huyo angepewa mkono wa Thank You ndani ya kikosi cha Yanga kwa kuwa alikuwa hajaripoti kambini huku mkataba wake wa mwaka mmoja ukiwa umegota mwisho na mazungumzo yalikuwa yanatajwa kusitishwa kwa muda.

Julai 12 Mkude aliwasili kambini na kuanza mazoezi pamoja na wachezaji wengine ambapo anakutana na kiungo Clatous Chama waliyewahi kucheza pamoja ndani ya Simba.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga aliweka wazi kuwa Mkude bado ni mchezaji wa Yanga na hawana mpango wa kuachana na mchezaji mzuri.

“Jonas Mkude ni mchezaji wa Yanga, walipoona kwenye ufukwe kwamba hayupo sijui fulani mara jezi namba 20 imekuaje hapana Mkude ni mchezaji wa Yanga.”