>

SIMBA KUANZA NA MMOJA KATI YA UHAMIAJI AU BINGWA WA FA LIBYA

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa Simba itakutana na mshindi wa mchezo  kati ya Uhamiaji ya Zanzibar au Bingwa wa FA ya Libya, Libya 1 kwenye raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/25.

Timu ya Uhamiaji ya visiwani Zanzibar imepangwa dhidi ya wawakilishi hao kutoka Libya katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali CAFCC ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atakutana na Mnyama kwenye raundi ya kwanza.

Ipo wazi kwamba Simba ambayo imeweka kambi nchini Misri haitaanzia kwenye hatua ya awali hivyo itakuwa ikimsubiri mshindi mmoja kwenye mchezo huo kupambana naye.

Wanamangush, Coastal Union ya Tanga watakabiliana na FC Bravos ya Angola kwenye hatua ya awali ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atachuana na Fc Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Timu mbili kutoka Tanzania zitapeperusha bendera kwenye anga la Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ni Simba iliyogotea nafasi ya tatu na Coastal Union iliyogotea nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu Bara.

Yanga na Azam FC hizi timu mbili zitakuwa kwenye anga la kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na zote zitaanzia hatua ya awali ambapo Julai 11 2024 droo ilichezwa nchini Misri na kila timu ikamtambua mshindani wake.