>

BOKA ATUA YANGA KUZIBA PENGO LA JOYCE LOMALISA

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi hawana jambo dogo kwa kuwa wameamua kufanya maboresho katika kikosi hicho.

Ipo wazi kwamba timu hiyo kwenye mechi zake zote za nyumbani haikupoteza ikiwa ni rekodi kubwa ndani ya msimu uliogota mwisho ikiwa na pointi 80 kibindoni.

Nyota mwingine ambaye ameongezwa ndani ya kikosi cha Yanga ni beki wa kushoto, Chadrack Boka (24) raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutoka FC Saint Lupopo ya nchini kwao kwa mkataba wa miaka miwili utakaombakisha Yanga mpaka 2026.

Beki huyo ambaye amekuwa akijumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya DRC anatua Jangwani kuziba pengo la Joyce Lomalisa ambaye ameoneshwa mlango wa kutokea.

Hivyo beki huyo anatarajiwa kuwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa msimu mpya wa 2024/25 ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kupambania kombe.