KOCHA Mkuu wa Geita Gold, Dennis Kitambi ameweka wazi kuwa anatambua mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba utakuwa na ushindani mkubwa lakini wapo tayari kusaka pointi tatu muhimu.
Mchezo huo ni mzunguko wa pili ambapo kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 ubao ulisoma Geita Gold 0-1 Simba.
Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 60 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 27 inakutana na Geita Gold ambayo imecheza mechi 27 kwenye msimamo ipo nafasi ya 15 na pointi 25.
Kitambi amesema: “Natambua mchezo utakuwa ni mgumu na wenye ushindani mkubwa lakini tumefanya maandalizi vizuri tunatambua namna ya kuwakabili wapinzani wetu Simba.
“Sikupata muda wa kuwafuatilia kwenye mechi zao za hivi karibuni lakini tutahitaji kufanya vizuri kwenye mchezo wetu kwa kutawala katika umiliki pamoja na kutengeneza nafasi nyingi na kuzitumia.”
Mchezo huo wa ligi unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Mei 21 ikiwa ni mzunguko wa pili.
Mchezo uliopita kwa Geita gold iligawana pointi mojamoja kwa kutoshana nguvu bila kufungana na Coastal Union ya Tanga.