LEGEND kwenye upande wa uandishi wa Habari za Michezo na Burudani Bongo, Saleh Ally, Jembe ameweka wazi kuwa timu ya taifa ya Tanzania ya Taifa Stars inazidi kuimarika taratibu na mechi za kirafiki zitakuwa na faida hapo baadaye kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Jembe amebainisha kuwa licha ya Stars kuanza kwa kuchechemea kwenye mchezo wa kirafiki kwa kupoteza bado kuna nafasi ya kufanya vizuri siku zijazo kutokana na uhalisia wa wachezaji kuwa na ari ya kujituma.
“Timu ilifika siku tano zilizopita na ilicheza dhidi ya Sudan tukapoteza kwa kufungwa 2-1 kwenye mchezo huo ambao Stars ilianza kwa kucheza chini kutokana na kutoelewana kwa kuwa wachezaji wengi walikuwa hawajacheza pamoja kwa muda mrefu lakini taratibu walizidi kuwa imara.
“Kuna mchezo mmoja Jumapili baada ya hapo itakuwa na safari ya kurejea Tanzania, Ally Salim alianza kucheza kwenye mchezo wa kwanza na mabao yote ilikuwa ni aina moja.
“Mpira umepigwa kona hakuna wa kuokoa mpira tukafungwa, dakika 15 za mwisho wachezaji wa Tanzania waliamka na walicheza kwa juhudi jambo ambalo liliwafanya wachezaji wa Sudan kuanza kupoteza muda.
“Kikosi cha Tanzania kimekuwa na sura nyingi mpya ikiwa ni pamoja na Jabir Mpanda ambaye anaandika rekodi yakucheza akiwa na miaka 17 tu ni njia nzuri kwa ajili ya kujenga kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania.
“Kwa TFF naona wanafanya jambo zuri kila sehemu wameanza sasa maandalizi huenda Watanzania wanaweza wasifurahi kwa kuwa kutakuwa na maumivu kwa kuwa matokeo yatakuwa hayapatikani bali maandalizi kwa timu husika.”