INAELEZWA kuwa kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge anatajwa kuja kuchukua mikoba ya Abdelhak Benchikha ambaye amebwaga manyanga ndani ya kikosi hicho.
Kwa sasa Simba inanolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda akishirikiana na Seleman Matola ambapo mchezo wao ujao ni dhidi ya Dodoma Jiji unatarajiwa kuchezwa Mei 17 2024 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Kocha huyo amesema itakuwa ni heshima kwake endapo atapata nafasi ya kuinoa timu mojawapo za Ligi Kuu Tanzania haswa Simba yenye nafasi ya kuwania mataji na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ibenge ambaye ni maarufu kwa mashabiki wa Tanzania, alisema bado ana mkataba wa mwaka mmoja na waajiri wake Al Hilal lakini ikitokea nafasi ya kufundisha Tanzania itakuwa ni heshima kubwa kwake.
Siyo mara ya kwanza Ibenge kutajwa Simba kwani tangu alipokuwa akiinoa AS Vita, viongozi wa Wanamsimbazi walionyesha hamu ya kuhitaji huduma yake ingawa mara zote kikwazo kimekuwa kikitajwa kuwa ni mshahara mkubwa ambao hauendani na uhalisi wa uchumi wa klabu za Tanzania.
“Nimeshafundisha nchi nyingi kwa mafanikio nafikiri ikitokea nikapata nafasi ya kuja kufundusha Tanzania itakuwa ni heshima kwangu na naamini pia nitakuwa na muendelezo mzuri kwenye CV yangu,” alisema Ibenge ambaye analijua vyema soka la Tanzania na huenda klabu yake ya Al Hilal ikacheza ligi hiyo msimu ujao kama sehemu ya kujiweka fiti.