ANAITWA Jabir Seif Mpanda ameandika rekodi ya kuitumikia timu ya soka ya taifa ya Tanzania Taifa Stars akiwa amekamilisha miaka 17 na siku 98.
Rekodi inayoonyesha kuwa mchezaji mdogo zaidi kuitwa kwa mara ya kwanza na kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Taifa Stars.
Jabir anayekipiga katika timu ya U17 ya Getafe ya Hispania ameitwa katika kikosi cha Stars chini ya Kocha Hemed Seleman Morocco.
Aliingia katika kipindi cha pili katika dakika ya 78 akichukua nafasi ya Ben Starke.
Tokea ameingia Jabir alifanikiwa kugusa mpira mara 14 huku Stars ikionekana kuwazidia wenye wao kwenye Dimba dogo la King Fahad mjini Taif nchini Saudi Arabia.
Jabir ni kati ya vijana wa Kitanzania wanaochipukia wakiwa na malezi ya soka katika nchi za England na Hispania.
Kijana huyo kutoka familia ya Mpanda ni mkubwa na ana wadogo zake wawili Tariq na Barka ambao wote wanacheza soka nchini Spain.
Rekodi imeandikwa, kila la kheri Jabir katika kutimiza majukumu yako kila wakati.