AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa wanatambua ugumu uliopo kwenye mashindano wanayocheza lakini wapo tayari kuona kwamba wanashinda mchezo huo ambao ni muhimu kwao.
Simba inapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya makundi ambapo kuna timu mbili kutoka Tanzania.
Yanga wao watakuwa na kazi dhidi ya Mamelodi Sundowns mchezo unaotarajiwa kuchezwa Machi 30 Uwanja wa Mkapa.
Ally amesema: “Simba ya kwenye makundi sio Simba itakayocheza robo fainali. Itakuwa Simba mpya, Simba ya kuitaka nusu fainali. Hii mechi ndio itakuwa mechi bora wa hatua ya robo fainali sababu inamkutanisha bingwa mtetezi na timu namba tano bora barani Afrika.”
“Nichukue nafasi hii kwa unyenyekevu kuwakaribisha na kuwaita Uwanja wa Mkapa siku ya tarehe 29. Ni mechi ambayo inatuhusu sana mashabiki wa Simba. Tumecheza mechi nyingi ya robo fainali lakini hii ndio robo fainali bora zaidi. Yani kama hauji kuona mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly jiulize mechi gani utakuja uwanjani.
“Sisi tunaamini mara mbili zote ambazo tumemfunga Al Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa ni kwa sababu ya mashabiki hivyo silaha namba moja ni mashabiki. Mkija uwanjani tukaujaza uwanja tutamfunga vizuri na hilo tumeshathibitisha. Siri ya ushindi ni wewe Mwanasimba. Tukumbuke ya kwamba hatuhitaji tu ushindi, tunahitaji ushindi mkubwa wa kutupeleka nusu fainali.
“Safari hii tunataka kupata ushindi mkubwa wa kutupeleka nusu fainali, tukishinda goli nyingi Uwanja wa Mkapa tukienda kwao hata tucheze siku tatu hawatakuwa na uwezo wa kupindua matokeo.
“Tarehe 29 ni siku ya kufa na kupona, siku ya kupambania Simba yetu. Tujitahidi kila Mwanasimba aje Uwanja wa Mkapa. Tuhamasishane kwenye matawi, kwenye makundi, kwenye mitaa ili tarehe 29 tukutane Uwanja wa Mkapa.
“Mechi yetu ni saa 3 usiku hivyo una option ufturu nyumbani ndio uje uwanjani, au uje Uwanja wa Mkapa utafturu huko huko, itauzwa nje ya uwanja alafu ndio uingie uwanjani. Huna sbabau yoyote ya kutokuja uwanjani siku hiyo.
“Tupo kwenye mazungumzo na Jeshi la Polisi ili kuwe na ruti ya magari kuja moja kwa moja uwanjani. Tunaongea nao pia usalama uwe madhubuti, mara nne ya zile mechi za mchana ili Wanasimba waje uwanjani na waondoke uwanjani kwa usalama. Uzuri tunae Afande Mudi ni Mkuu wa Kituo cha Chang’ombe ambaye atahakikisha Mwanasimba hapati madhara yoyote.
“Wewe mwenyewe hapo ulipo jiambie unatakiwa kwenda uwanjani, weka nia. Na tiketi zimeanza kuuzwa, hii ni mara ya kwanza tiketi kuanza kuuzwa wiki moja na nusu kabla kutokana na umuhimu na uhitaji wa tiketi kwa Wanasimba,”.