TIMU ZILIZOFUZU ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA ULAYA

Hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imekamilika huku wababe 8 wa Ulaya wakitinga robo fainali.

Atletico Madrid na Borussia Dortmund zimeungana na Real Madrid, Manchester City, Barcelona, Arsenal, Bayern Munich na PSG kwenye hatua hiyo kufuatia ushindi usiku wa kuamkia leo.

Atletico Madrid imefikia hatua hiyo baada ya ushindi wa penalti 3-2 dhidi ya Inter Milan baada ya ushindi wa 2-1 kulazimisha mchezo kuamuliwa kwa matuta. Itakumbukwa Inter Milan ilishinda 1-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa 16 bora.

Kwingineko, mabao ya Jadon Sancho na Marco Reus yaliipeleka Borussia Dortmund kwenye robo fainali kufuatia ushindi wa 2-0 ikiwa ni ushindi wa jumla wa 3-1 dhidi ya PSV ya Uholanzi.

Droo wa hatua ya robo fainali itafanyika kesho Ijumaa, Machi 15, 2024 mjini Nyon, Uswisi ambapo wababe hao watabaini wapinzani wao.