YANGA YAWASILI MISRI KUWAKABILI WAARABU

MSAFARA wa kikosi cha Yanga inayofundishwa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kimewasili salama nchini Misri kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hiyo inatarajiwa kuvaana na Waarabu wa Misri Al Ahly kwenye mchezo wa mwisho wa kundi D na timu zote zina uhakika wa kuwa ndani ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni jioni ya Februari 27 msafara wa Yanga uliojumuisha wachezaji 24 pamoja na viongozi ulianza safari na mapema Februari 28 wametia timu salama nchini Misri.

Mchezo huo wa Yanga dhidi ya Al Ahly unatarajiwa kuchezwa Machi Mosi 2024 ambao ni wa hatua ya makundi ukiwa ni mchezo wa sita.

Yanga imetinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi 8 kibindoni.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.